Maswaaba
Ni
mmoja kati ya watu wanane wa mwanzo kusilimu. Pia ni miongoni mwa watu
kumi walibashiriwa pepo na Mtume (SAW). Alikuwa mmoja kati ya watu
sita waliochaguliwa na Umar kuunda baraza la ‘Shura’ kumchagua Khalifa
baada ya kifo chake.
Jina
lake enzi za ujahiliya lilikuwa Abu Amr. Aliposilimu Mtume (SAW)
akamwita Abdulrahman (mja wa mwenye kurehemu). Alisilimu hata kabla
Mtume (SAW) hajaanza kwenda kwa Al-Arqam na inasemekana alisilimu siku
mbili tu baada ya kusilimu Abubakar Siddiq.
Abdulrahman
hakukimbia mateso na adhabu za Maquraysh. Alivumilia madhila na mateso
na kubaki na imani yake thabiti. Pale walipolazimika waislam kufanya
Hijira kwenda Habashah, Abdulrahman naye pia alikwenda. Alirudi Makka
baada ya kusikia uvumi kwamba hali za waislam zimekuwa nzuri na baada ya
kuthibitika kwama zilikuwa ni uzushi tu, alifanya tena Hijra kuelekea
Habashah na alihitimisha kwa hijra ya Madina.
Punde
tu, alipowasili Madina. Mtume (SAW) aliwaunganisha Muhajirin na
Ansaar. Lengo la udugu huu lilikuwa kuweza kuwa na maelewano ya kijamii
na pia kuwapunguzia ukiwa muhajiruun. Abdulrahman akakutanishwa na
Saad ibn Ar-Rabiah. Baada ya kuatambulishwa rasmi, Saad akamwambia
Abdulrahman:
“Ndugu
yangu, mimi ndiye mwenye utajiri mkubwa hapa Madina, nina vikataa
viwili na wake wawili. Angalia ni kipi kati ya vikataa hivi viwili
utakipenda na nitakuachia na angalia yupi kati ya wake zangu
amekupendeza na nitampa talaka kwa ajili yako”
Abdulrahman hakutarajia yote haya kwani alionekana kidogo kuingiwa na aibu na kujibu:
“Inshaallah
Mwenyezi Mungu akurehemu katika familia yako na utajiri wako.
Tafadhali kwa hisani yako nioneshe soko tu liko wapi?”
Abdulrahman
alioneshwa soko na kuanza biashara kwa kile kichache alichokuwa nacho.
Akafanya biashara na kupata faida haraka. Muda mchache tu hali yake
ikawa nzuri sana kibiashara akajitafutia mke na kuoa.
Siku moja, alikwenda kwa Mtume (SAW) huku akinukia uturi na manukato:
“Maliyam!,
ewe Abdulrahman! Akasema Mtume Muhammad (SAW) kwa mshangao. (maliyam ni
neno la asili ya kiyemen linaainisha mshangao).”
“Nimeoa,” akajibu Abdulrahman.
“Na mkeo ulimpa kitu gani kama mahari yake?”
“Uzito wa ‘uwat’ wa dhahabu”
“Lazima
ulishe walima hata kama ni kondoo mmoja na Mwenyezi Mungu (SW)
akubariki katika utajiri wako,” akamalizia Mtume (SAW) huku akitabasamu.
Abdulraham
alipigana vita vya Badr na Uhud kwenye vita vya Uhud alisimama imara
licha ya kuwa na majeraha karibu ishirini mwilini mwake na mengine ya
kutisha. Jitihada yake ya nafsi ilikwenda sambamba na jihadi yake ya
mali.
Kuna siku moja, Mtume (SAW) alikuwa akijiandaa kutuma jeshi vitani na akalihutubia kwa kusema:
“Toeni sadaka kwani ninataka kulituma jeshi.”
Haraka
haraka Abdulrahman alikwenda nyumbani kwake na kurudi, “ewe mjumbe wa
Mwenyezi Mungu; akasema, nina (dinar) elfu nne. Ninatoa elfu mbili kama
mkopo kwa mola wangu na kuiachia familia yangu zilizobaki.”
Mtume
(SAW) alipoamua kutuma jeshi Tabuk ambapo kulikuwa mbali sana. Haja ya
msaada wa fedha ilikuwa kubwa kama ilivyokuwa haja ya wana jihadi.
Kwani majeshi yao yalikuwa yameandamana vyema na kuwa na zana nzito za
kivita.
Mwaka
huo Madina kulikuwa na njaa na ukame. Safari ya Tabuk ilikuwa ndefu na
zaidi ya kilomita elfu moja. Chakula hakikutosha na usafiri ulikuwa
mchache mno mpaka Mtume (SAW) kuwarudisha kundi la waislam waliokuwa
tayari kwa vita kwa kukosekana usafiri.
Waislam
walioachwa nyuma walisikitika sana na wakajaeleweka kama ‘Bakkaa-in’
waliokuwa wakilia. Na jeshi hili likaitwa jeshi la Usrah- ‘taabu’.
Hapo Mtume (SAW) akawahimiza masahaba watoe walichonacho kwa moyo mmoja
kulisaidia jeshi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuwahakikishia malipo
makubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Naam!
Wito ukaitikiwa na waislam wakajitolea kwa wingi na miongoni mwao ni
Abdulrahman. Alitoa wakia mia mbili za dhahabu na hapo Umar ibn Khattab
alisema:
“Sasa nimemuona Abdulrahman anafanya kosa, hukuiachia chochote familia yake.”
“Umeiachia chochote familia yako, Abdulrahman?” Mtume (SAW) alimuuliza.
“Ndio, nilichowaachia ni kingi kuliko nilichotoa na ni bora,” akajibu Abdulrahman.
Mtume akauliza, “kiasi gani?”
“Kile ambacho Mwenyezi Mungu na Mtume wake ameahidi navyo ni rizki, mambo mema na malipo.”
Jeshi
la waislam likaanza safari kuelekea Tabuk. Abdulrahman akabahatika
kupata heshima ambayo kabla yake hajawahi kupewa mtu yoyote. Ulipofika
wakati wa sala na Mtume (SAW) hakuwepo wakamchagua Abdulrahman kuwa
Imam. Mtume (SAW) alipodiriki sala, tayari rakaa ya kwanza ilikwisha
malizika na akasali maamuma. Je! Kuna hadhi imam wa Al-habib Mustafa
(SAW), kiumbe kilicho bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu, imam wa Mitume yote
Muhammad alayhi ssalaatu wassalam!
Mtume
Muhammad (SAW) alipofariki, Abdulrahman alichukua jukumu la kuihudumia
familia yake, Ummahatul Muuminiin. Aliwashughulikia kwa mahitaji yao na
kwenda nao Hija pamoja ili kuhakikisha mahitaji yao yametimizwa. Huu
ni uaminifu ambao alipata katika familia ya Mtume (SAW).
Aliwahi
kuuza sehemu ya ardhi kwa dinar elfu arubaini na kuzigawa zote kwa Banu
Zahrah jamaa wa mama yake Mtume (SAW), wakeze Mtume (SAW) waliokuwa
masikini. Na Bi Aisha (RA) alipopata mgao wake aliuliza:
“Ni nani aliyeleta fedha hizi?
Akaambiwa ni, “Abdulrahman.”
Mtume amesema, “hakuna mtu yoyote atakayewaonea huruma nyinyi baada ya kufa kwangu isipokuwa wale walio na subira.”
Dua
za Mtume (SAW) zilikubalika kwani Abdulrahman Ibn Awl alikuja kuwa
tajiri mkubwa miongoni mwa masahaba wa Mtume (SAW), makundi yake ya
misafara toka na kuja Madina yalizidi kukua siku hadi siku. Aliwaletea
watu wa Madina unga, ngano, samli, nguo, vyombo vya kupikia, manukato na
chochote kitakachohitajika na kuuza nje bidhaa zilikuwa zikizalishwa.
Siku
moja, sauti kubwa ikasikika ikitokea nje ya mipaka ya mji wa Madina,
mji ambao kwa kawaida ni tulivu sauti ilizidi kuongezeka huku mawingu ya
vumbi na michanga yakirushwa juu angani. Wakagundua kwamba ni kundi
kubwa la ngamia takriban mia saba huku limesheheni mizigo linaingia
Madina. Watu wakawa wanaitana kuja kushuhudia ni bidhaa gani msafara
huu wa ngamia wote hawa umeleta:
Bi Aishah, akasikia zogo lile na akauliza, “nini tena hiki kinachotokea Madina?
Akaambiwa, “ni msafara wa Abdulrahman ibn Awl unatoka Syria na bidhaa”
“Msafara tu ndio unaofanya zogo lote hili?” Akauliza huku haamini.
“Naam, Yaa Ummul Muuminiin, wapo ngamia mia saba”
Bi
Aisha akatikisa kichwa chake na akashika tamaa kama aliyepigwa na
butwaa kama kwamba anajaribu kukumbuka tukio au jambo lililopita kasha
akasema:
“Nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu akisema, nimemuona Abdulrahman Ibn Awl anaingia peponi, huku akitambaa.”
Kwa nini atambae? Kwa nini haingii mara moja kwa kuruka pamoja na masahaba wa mwanzo wa Mtume (SAW).
Baadhi
ya masahaba wake wakamhadithia Abdulrahamn riwaya hii. Akakumbuka
alishawahi kuisikia hadithi hii zaidi ya mara moja kutoka kwa Al-habib
Mustafa (SAW) na akaharakiza kuelekea kwa Bi Aisha na akamwambia: “Yaa
Ammah! Ewe mama yangu! Umeyasikia haya kutoka kwa Mtume (SAW).
“Ndio,” akajibu.
Abdulrahman akafurahi sana na akaongezea:
“Kama
ningeliweza ningeliingia peponi huku nimesimama. Nnakuapia yaa Ammah,
msafara wote huu na bidhaa zake zote ninautoa fi Sabiili Llah!
Hilo alilitekeleza kwa ukarimu huu aliounesha na uadilifu na kuwagawia watu wa Madina na vitongoji vyake.
Hili
ni tukio moja tu linalomuonesha Abdulrahman kuwa ni mtu wa aina gani?
Alipata utajiri mkubwa lakini haukumvaa wala hakuuvaa.
Aliendelea
kutoa kwa mikono yuke yote miwili kwa siri na kwa dhahiri. Na baadhi
ya misaada aliyoitoa, dirham elfu arubaini, dinar elfu arubaini. Wakia
mia mbili za dhahabu, farasi mia tano kwa mujahidina, dinar mia nne kwa
waliopona vita vya Badr na sehemu kubwa aliyoitoa kwa wake za Mtume
(SAW) na bado listi inaendelea……
Na kwa ukarimu wake Bi Aisha alisema:
“Inshallah Mwenyezi Mungu (SW) amnywishe kwenye chemchem ya Salsabil.”
Utajiri
wote huu haukumtia jeuri wala kiburi na haukumbadilisha chochote.
Alipokuwa na wafanyakazi na wasaidizi wake hawezi kumtofautisha
kabisa. Siku moja aliletewa chakula kufutari, alikitazama kasha
akasema;
“Musab
ibn Umayr aliuwawa, yeye alikuwa bora kuliko mimi. Hatukuwa na hata
guo la kumsitiri tukimfunika kichwani miguu huwa wazi, kisha Mwenyezi
Mungu (SW) akatujaalia rizki hizi za kidunia………nina wasi wasi kwamba
malipo yetu tayari tumeshalipwa mapema duniani.” Akaanza kulia na
kushindwa kula.
Na Inshallah Mwenyezi Mungu amuweke Abdulrahman katika kundi la wale…… Suratul Baqarah 262.
No comments:
Post a Comment