Dunia imekamilika
Mwezi
wa Dhul Hijja ni katika miezi iliyotukuzwa na Mwenyezi
Mungu Subhanahu wa Taala.
Mwenyezi
Mungu anasema;
“Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi
Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukmu ya Mwenyezi Mungu tangu alipoumba
mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitukufu (kabisa).
Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi
msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na
washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi
nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachaMungu”.
“Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni
kuzidi katika kukufuru; kwa hayo, hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka
mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa
sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa
hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu makafiri”.
At Tawba – 36 – 37
Wakiisogeza miezi
Katika
kuzifasiri aya hizi, Sheikh Abdulla Saleh Farsy (Mwenyezi Mungu amrehemu)
amesema:
“Nabii
Ibrahimu na Nabii Ismail waliwafundisha Waarabu kuihishimu sana sana miezi
minne hii ;
Dhul Qaedah
(Mfunguo pili) –
Dhul Hijjah (Mfunguo
tatu) -
Muharram (Mfunguo nne) na
Rajab wasifanye jambo lolote baya, khasa
kupigana (Vita). Lakini karne nyingi zilipopita waliionea
uzito sharti hii ya kutopigana. Basi wakaanza kufanya ujanja wa kuikimbia kimbia. Wakaanza kuisogeza
miezi ya mwaka. Badili ya kuwa mwaka mmoja una miezi kumi na mbili wakaifanya miezi kumi na tatu au zaidi ili ikawie
kufika ile miezi mine inayokatazwa kupigana ndani yake.
Kwa
hivyo kila mwaka wanapokutana Makka siku ya Arafa mmoja katika wakubwa wao
(Mkubwa wa makabila ya Kiarabu) huinuka na kutoa
habari kuwa mwaka huo mpya ujao waufanye mezi kumi na tatu au kumi na nne, kwa
kuihisabu mara mbili baadhi ya ile miezi isiyokatazwa kupiganwa. Kama kusema:
“Ukiandama
Mfunguo nne uliotukabili tuwite mwezi mpya; ‘Mfunguo
tano wa mwanzo,’ na wa pili wake tuwite; ‘Mfunguo tano wa pili,” badala ya
kuuwita Mfunguo sita.
Tena
wa tatu ndio wauwite Mfunguo sita, ili miezi minne (iliyoharamishwa
kupigana) ikawie kufika.
Ndio
Mwenyezi Mungu anawalaumu hapa na kuonyesha kuwa japo
wanaitukuza miezi minne katika mwaka, lakini miezi minne la haiwi thuluthi ya
mwaka kwani mwaka wanauzidisha miezi mingine kusudi, ili ikawie kufika”
(Mwisho
wa maneno ya Sheikh Abdullah Saleh.
Kutoka
kwa Abibakra Nafiu bin Al Harith (Radhiya Llahu anhu)
amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alipowahutubia
Waislamu katika Hija yake ya mwisho ‘Hijjatul Wida'a’, alisema:
“Hakika
dunia imekamilika kama
ilivyokamilika siku ile Mwenyezi Mungu alipoziumba mbingu na ardhi. Mwaka una
miezi kumi na mbili. Ndani yake imo (miezi) minne
Mitukufu, mitatu imekamatana Dhul Qaeda, Dhul Hijja na
Muharram. Na Rajab (upo peke yake) baina ya Jamaad na
Shaabani. Huu (mwezi tulio ndani yake) ni mwezi gani?”
Tukasema;
“Mwenyezi
Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi”
Akanyamaza, hata tukadhani kuwa labda
ataubadilisha jina.
Kisha
akauliza:
“Huu
si mwezi wa Dhul Hijja?”
Tukamjibu:
“Ndiyo”
Akauliza:
“Mji gani huu?”
Tukasema:
“Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi.”
Akanyamaza
hata tukadhania kuwa labda ataubadilisha jina lake.
Kisha
akasema: “Huu si Mji (Mtukufu)?”
Tukamjibu:
“Ndiyo.”
Kisha
akauliza: “Siku gani hii?”
Tukamjibu:
“Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi”
“Si siku ya Al Nahr hii (Siku kuu mosi kubwa)?”
Tukamjibu:
“Ndiyo.”
Akasema:
“Hakika
damu zenu na mali
zenu na heshima zenu ni tukufu baina yenu kama
ulivyo utukufu wa siku hii yenu katika mji huu wenu katika mwezi huu wenu. Na
Mtakuja kuonana na Mola wenu na atakuulizeni juu ya
amali zenu, basi msije mkarudi baada yangu (baada ya kufa kwangu) mkawa
makafiri mnakatana shingo wenyewe kwa wenyewe. Aliyehudhuria amjulishe
asiyehudhuria…”
Kisha
akasema:
“Si nimefikisha?”
Tukasema:
“Ndiyo”
Akasema:
“Mwenyezi
Mungu shuhudia”
Bukhari
na Muslim
Sababu za kutukuzwa
Kalenda
ya Kiislam (Al Hijri) ina miezi kumi na miwili
sawa na kalenda ya Gregory, isipokuwa majina ya miezi yake
inakhitalifiana, na idadi ya siku chache pia inakhitalifiana.
Yafuatavyo
ni majina ya miezi ya kalenda ya Kiislamu (Al Hijri):
Miezi
mitukufu nimeiandika kwa herufi kubwa:
1. MUHARRAM (Mfunguo nne)2. Safar3. Rabiul Awwal (Mfunguo sita)4. Rabiul Thani5. Jamadul Awwal6. Jamadul Thani7. RAJAB8. Shaaban9. Ramadhan10. Shawwal11. DHUL QAEDA (Mfunguo pili)12. DHUL HIJJA (Mfunguo tatu)
Maulamaa
wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ameiteuwa miezi minne hiyo kuwa mitukufu na kukataza watu kupigana vita ndani yake kwa sababu maalum;
nayo ni kuwawezesha watu kwenda Makka kufanya Ibada ya Hija na ya Umra kwa amani
na kurudi makwao kwa amani.
Ameuteuwa
mwezi wa Dhul Qaeda (Mfunguo pili) ulio kabla ya mwezi
wa Dhul Hijja (Mfunguo tatu), ili watu waweze kusafiri kutoka makwao kuelekea
Makka bila ya kudhuriwa. Na akauchagua mwezi wa Dhul
Hijja kwa ajili ya kuifanya ibada hiyo ya Hija kwa amani. Kisha akautukuza
mwezi wa Muharram ili watu baada ya kuhiji waweze
kurudi makwao kwa amani.
Ama
mwezi wa Rajab ulio kati kati ya mwaka, Mwenyezi Mungu
ameutukuza kwa ajili ya kuwawezesha watu kwenda Makka kuizuru nyumba, na kwa
ajili ya kufanya Umra.
Kisha
Mwenyezi Mungu akasema:
“Hiyo
ndiyo Dini iliyo sawa”
Na
maana yake ni kuwa huo ndio mwenendo ulio sawa wa
kuiheshimu miezi hiyo na kutopigana vita ndani yake kama
anavyokutakeni Mola wenu.
Kisha
akamalizia kwa kusema:
“Basi msidhulumu nafsi zenu humo”.
Na
maana yake ni kuwa; msidhulumu nafsi zenu katika miezi
hii minne ambayo ni mitukufu, na hasa katika mji mtukufu au kwa kuwafanyia
maovu wale waendao kufanya ibada hii tukufu.
Msidhulumu nafsi zenu
Wafasiri
wengine wamesema kuwa maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala:
”Msidhulumu
nafsi zenu”, Ni katika miezi yote kumi na miwili,
isipokuwa katika miezi minne hiyo dhambi zake huwa kubwa zaidi.
Imam
Shafi na baadhi ya maulamaa wanaona kuwa malipo ya
Fidya katika miezi hii ni kubwa zaidi kupita katika miezi mingine kutokana na
ukubwa wa dhambi ndani yake.
Ama
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) akiifasiri aya hii alisema:
“Basi
msidhulumu nafsi zenu humo,” ni katika miezi yote, kisha Mwenyezi Mungu akaihusisha miezi
minne hiyo, akaitukuza na kulifanya tendo la dhambi katika miezi hiyo kuwa ni
kubwa na matendo mema pia ujira wake akaufanya kuwa ni mkubwa”.
Ama
Qatada yeye anasema:
“Hakika
ya dhulma na dhambi katika miezi mitukufu malipo yake
ni makubwa zaidi kupita katika miezi mingine, ingawaje dhulma kwa vyovyote
dhambi yake ni kubwa sana.
Lakini Mwenyezi Mungu hutukuza na kuteua anavyotaka.
Mwenyezi Mungu ameteuwa na kuvitukuza vingi katika
viumbe vyake. Ametukuza miongoni mwa Malaika akawajaalia wengine kuwa ni
wajumbe, na katika wanadamu pia akawateuwa wengine kuwa Mitume, na katika
maneno, ameteuwa utajo wa Mwenyezi Mungu Dhikri, na katika ardhi,
akateuwa misikiti kuwa ni mwahali bora, akateua katika miezi mwezi wa Ramadhani
pamoja na miezi hiyo Mitukufu kuwa ni bora, na katika siku akaiteuwa siku ya
Ijumaa na katika usiku ameuteuwa usiku wa Laylatul Qadr, kwa hivyo tukuzeni
yale aliyoyatukuza Mwenyezi Mungu, na hayatukuzi yale aliyoyatukuza
Mwenyezi Mungu isipokuwa mwenye kufahamu na mwenye akili”.
Mwenyezi
Mungu anasema:
“Enyi mlioamini! Msivunje hishima ya
alama za (dini ya) Mwenyezi Mungu wala (hishima) ya mwezi uliotukuzwa….”
Al
Maidah – 2
Wanakuuliza
Masahaba
(Radhiya Llahu anhum) walipigina na makafiri waliokuwa
wakiongozwa na Amru bin Al Hadhramiy huko Taif, wakidhani kuwa siku hiyo
ilikuwa ni usiku wa mwisho wa mfunguo tisa (tarehe 30 Jamadul thani). Hawakujua
kuwa mwezi wa Rajab ambao ni katika miezi mitukufu
umekwishashaingia.
Amru
bin Al Hadhramiy aliuliwa, na Waislamu wakateka kila kilichokuwemo ndani ya msafara wa
makafiri hao.
Makafiri
wakaenda kumsikitikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam) na kumlaumu kuwa amevunja heshima ya miezi mitukufu.
Ndipo
Mwenyezi Mungu alipowateremshia aya zifuatazo kuwafahamisha kuwa kupigana vita
katika miezi hiyo ni dhambi kubwa sana, lakini yale wanayofanya wao katika
kuwatesa, kwauwa na kuwazuwia Waislamu wasiilinganie dini ya Mwenyezi Mungu,
dhambi yake ni kubwa zaidi.
Mwenyezi
Mungu anasema:
“Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi
mtakatifu.
Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini
kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na
kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa
watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi
mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama
wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika
duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo
watadumu.”
Al Baqarah – 217
Ibada ndani yake
Kutoka
kwa Abu Hurairah (Radhiya Llahu anhu) amesema:
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam) aliulizwa;
“Swala ipi iliyo bora baada ya zile za fardhi?”
Akajibu:
“Sala katika usiku wa manane.”
Kisha akaulizwa:
“Saumu ipi iliyo bora baada ya funga ya
Ramadhani?”
Akajibu:
“Mwezi mnaouita Muharram”.
Muslim na Abu Daud.
Mtu mmoja kutoka mji uitwao Baahila alimwendea Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) na kumuambia:
“Ewe Mtume Wa
Mwenyezi Mungu, mimi ni yule mtu aliyekujia mwaka uliopita”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam) akamuuliza:
“Nini kilichokufanya ubadilike hivi, kwani ulikuwa na umbile
zuri?”
Akasema:
“Sikuwa nikila chakula isipokuwa usiku tu tokea siku ile
tulipoachana”
(na maana yake ni kuwa mwaka mzima
alikuwa kila siku akifunga).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah
Llahu alayhi wa Sallam) akamuuliza:
“Kwa nini umejiadhibisha nafsi yako
hivi?”
Kisha akamuambia:
“Funga Mwezi wa Subira (Ramadhani), kisha
funga siku moja kila mwezi”.
Yule mtu akasema:
“Niongezee, kwani ninao uwezi wa kufunga
zaidi”.
Akamuambia:
“Funga siku mbili.”
Akasema: “Niongezee”
Akasema:
“Funga katika miezi mitukufu uache, funga katika miezi
mitukufu uache”,
huku akiashiria vidole
vitatu kisha akivikunja. (akimjulisha kuwa ndani ya
Miezi mitukufu afunge siku tatu kisha ale siku tatu).
Abu Daud, Ibni Majah na Al Baihaqi.
Anasema
Sayid Sabeq mwenye kitabu cha Fiqhi Ssunah:
“Funga
ya Rajab ina fadhila zaidi kupita miezi mingine si kwa
sababu nyingine isipokuwa ni kwa kuwa mwezi huo ni katika ile Miezi mitukufu”.
No comments:
Post a Comment