• Breaking News

    Friday, 6 January 2017

    Kulipa Rakaa

    Suali;
    Vipi mtu anailipa raka-a aloisahau anapokuwa ndani ya Sala au akeshamaliza?

    Jawabu;
    Mtume (SAW) anasema;
    "Mmoja wenu akitia shaka katika Sala yake, akawa hana hakika amesali raka-a moja au mbili, basi atajaalia kuwa amesali raka-a moja (tu). Na akiwa hana hakika amesali raka-a mbili au tatu, basi atajaalia kuwa amesali raka-a mbili, na akiwa hana hakika amesali tatu au nne, basi atajaalia kuwa amesali raka-a tatu, kisha atasujudu sajda mbili akishamaliza kusali kabla ya kutoa salamu akiwa bado amekaa."
    Ahmed na Ibni Majah na Attirmidhiy.
    Na katika hadithi nyingine anasema Mtume (SAW);
    "Mmoja wenu akitia shaka katika Sala yake akawa hajui amesali (raka-a) ngapi, tatu au nne, basi aondoe shaka na ahesabu zile raka- ambazo ana hakika nazo (yaani tatu) kisha asujudu sajda mbili kabla ya kutoa salam. Ikiwa atakuwa amesali raka-a tano, basi (sajda) zitamtakasia Sala yake, na ikiwa amekamilisha nne basi (sajda) zitamdhalilisha shetani."

    NAMNA NA KULIPA RAKA-A
    Kutokana na haya tunaelewa kuwa raka-a iliyosahauliwa, au yenye kutiliwa shaka inalipwa kama ifuatavyo;
    Kwa mfano ikiwa mtu anasali sala yenye raka-a nne, na akishafika raka-a ya nne akatia wasi wasi ni raka-a ngapi amesali, tatu au nne, basi atajaalia kuwa amesali raka-a tatu zile alizo na uhakika nazo, kisha anaongeza ya nne na anapomaliza na kabla ya kutoka salamu anasujudu sajda mbili kisha anatoa salamu bila kusoma tahiyatu.
    Ipo hitilafu baina ya maulamaa. Wapo wanaosema kuwa sajda ni baada ya kutoa Salamu hasa kwa Imamu, kwani akisujudu baada ya salamu atawababaisha wanaosali nyuma yake wale waliochelewa kwa sababu watainuka mara baada ya kutoa salamu.

    Zipo dalili zinazotujulisha kuwa mtu anaweza kuilipa raka-a aliyoisahau au alizozisahau wakati wowote ule hata kama ataikumbuka baada ya kutoa salamu na baada ya kuzungumza, au hata kama ataikumbuka baada ya kurudi nyumbani au hata baada ya kupita muda mrefu.
    Na wengine wanasema kuwa ukishapita muda wa kiasi cha kusabih, basi itambidi azisali tena raka-a zote kwa ukamilifu.

    Imepokelewa kuwa siku moja Mtume (SAW) alisahau akapunguza katika sala ya raka-a nne akasali mbili tu kisha akatoa salamu. Mtu mmoja aitwae 'Dhul yadayni' akamuuliza;
    "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Umesahau au umepunguza kusudi katika Sala?"
    Mtume (SAW) akasema;
    "Sikusahau wala sikupunguza (kwa makusudi)."
    Kisha akawauliza Abubakar na Omar;
    "Ni kweli anayosema Dhulyadayani?"
    Wakasema;
    "Ni kweli."
    Mtume (SAW) akainuka na kuikamilisha Sala, kisha akatoa salamu, kisha akasema 'Allahu akbar', na kusujuu sajda mbili.
    Bukhari na Muslim

    No comments:

    Post a Comment

    Fashion

    Beauty

    Culture