Kabla
ya kusilimu kwake Ka’ab Ibn Malik alikuwa mmoja katika washairi wakubwa
katika mji wa Madina. Alijaaliwa ufasaha wa lugha ya kiarabu na
mashairi yake yalitumika katika vita vya Aws na Khazraj (Makabila mawili
makubwa katika mji wa Madina)
Sahaba Ka’ab ibn Malik, Allah Amuwie radhi, alishindwa
kuhudhuria vita vya Tabuuk pamoja na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam. Baadhi ya Masahaba walidiriki kutoa visingizio tofauti na
ilipofika zamu yake licha ya kuwa mfasaha wa maneno na mzuri katika
kujadiliana, alimwambia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam ukweli
kwamba ulikuwa ni uvivu na ajizi tu iliyomzuia na wala hana sababu
nyengine yoyote. Hata Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wassallam alisema baada
ya kumsikiliza: “Ama huyu amesema ukweli simama na ungojee mpaka Allah
Subhaanahu Wata’ala akuhukumie.”
Ka’ab
ibn Malik alisema ukweli. Lakini madhara yake yalikuwa makubwa. Mji
mzima wa Madina ulimgomea pamoja na wenzake wawili. Kwa takriban siku
hamsini hakuna aliesemezana nae wala kumjulia hali. Kisa alisema ukweli
mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ukweli ulimponza. Wale
waliodanganya mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam wakaonekana
ndio waungwana. Kwa mtazamo mfupi wa kibinadamu, kumeonekana uongo ndio
suluhisho.
Lakini
ukweli ulikuja kuthibitika kwamba athari zake zinakwenda mbali kuliko
uongo pale Allah Subhaanahu Wata’ala alipoteremsha aya kutoka kwake
inayowatakasa Ka’ab ibn Malik na wenzake . Attawbah/117- 118
لَقَد
تَّابَ الله عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ الَّذِينَ
اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ
فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ إِنَّهُ بِهِمْ رَؤُوفٌ
رَّحِيمٌ {117}
وَعَلَى
الثَّلاَثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُواْ حَتَّى إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ
الأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّواْ أَن
لاَّ مَلْجَأَ مِنَ اللّهِ إِلاَّ إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ
لِيَتُوبُواْ إِنَّ اللّهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ
Allah
amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari wali mfuata katika
saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi
akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye
kuwarehemu
Na
pia wale watatu walioachwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki juu ya
ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa
kumkimbia Allah isipokuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea kwa rehema yake
ili nao waendelee kutubu. Hakika Allah ndiye Mwenye kupokea toba na
Mwenye kurehemu.
Ka’ab
alitubu akarudi kwa mola wake pamoja na wenzake. Alisema kweli na
akajirudi kwa kosa lake. Athari zake ni kuteremshiwa wahy na Allah
Subhaanahu Wata’ala na kuuthibitishia ulimwengu (si mji wa Madina pekee
kwani Quraan inasomwa na itaendelea kusomwa mpaka siku ya kiama) kwamba
toba yao imepokelewa.
Licha ya kukubalika toba yake bado hakutosheka, Ka’ab alikwenda kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na kumwambia :
“Katika
toba yangu nilikuwa nijitakase kwa kuitoa mali yangu yote kwa ajili ya
Allah Subhaanahu Wata’ala na Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam”
Akasema Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam : “ Baki na baadhi ya mali yako ni kheri kwako”.
Akaendelea
kusema Ka’ab : “Ewe Mjumbe wa Allah! Hakika Allah ameniokoa kwa sababu
ya kuusema ukweli kwa hivyo katika toba yangu sitothubutu kusema uongo
ila nitakuwa mkweli katika umri wangu uliobakia.”
Ka’ab ibn Malik anathibitisha kauli kwa kusema: “Wallahi hakuna neema kubwa aliyonijaalia
Allah Subhaanahu Wata’ala baada ya kuniongoa kwa Uislamu zaidi ya kuwa
mkweli mbele ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam”
Naam
ni neema gani nyengine kama kila siku katika maisha ya ulimwengu Ka’ab
ibn Malik husomwa kila inaposomwa Suuratu Tawbah. Ni neema gani nyengine
kuliko kuthibitishiwa kukubaliwa toba kutoka kwa Allah Subhaanahu
Wata’ala. Ni aina gani ya toba ambayo licha ya kutubiwa bado Ka’ab
anataka kuitoa mali yake yote kama ni sadaka kwa ajili ya Allah na Mtume
wake. Ni kwa sababu ya kusema ukweli hata kama unauma, hata kama
utamdhuru, hata kama atakosa la kukosa almuradi wakati wa kutakiwa
kusema ukweli aliusema.
Ndio
maana Allah Subhaanahu Wata’ala baada ya kutukumbusha kisa cha Ka’ab na
wenzake pamoja na Waislamu walioshiriki katika vita vya Tabuuk ambao
walipata taabu na misukosuko ya aina yake akaendelea kwa kusema Attawbah
119
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ
Enyi mlioamini! Mcheni Allah, na kuweni pamoja na wakweli
Imaam
Ibn Kathiyr katika tafsiri yake anasema katika kuitafsiri aya hii
kwamba; semeni ukweli na mjiweke katika hali ya ukweli daima kwani
mtakuwa pamoja na wakweli na kuepukana na majanga na mabalaa na hatimae Allah kukupeni faraja.
Katika
hadithi nyengine Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema kama
ilivyopokewa na Abdullah ibn Masoud, Allah amuwie radhi:
“ Juu
yenu kusema ukweli kwani ukweli unakuongoza kwenye uadilifu na uadilifu
unakuongoza kwenye pepo. Hubaki mja anasema ukweli na hujichunga
kuusema ukweli mpaka huandikiwa mbele ya Allah kuwa ni Siddiyq – mkweli.
Na ole wenu na kusema uongo kwani uongo hukuongoza kwenye uovu na uovu hukuongoza kwenye moto. Hubaki mja anasema uongo na kujikita katika kusema uongo mpaka huandikwa mbele ya Allah – Muongo”. Bukhari na Muslim
No comments:
Post a Comment