• Breaking News

    Friday, 6 January 2017

    FAIDA anazopata mwenye kuzitunza SALA ZA ALFAJIRI NA ALASIRI


     
    Kumtii Mwenyezi Mungu
    Mwenyezi Mungu anasema;
    “Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.”
    Al Ahzab – 71

    Kuyashinda matamanio ya nafsi
    Mwenyezi Mungu anasema;
    “Na ama yule aliyeogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake, akaikataza nafsi yake na matamanio (maovu).
    Basi (huyo) Pepo ndiyo itakayokuwa makazi yake.”
    An Naziat – 40-41

    Kuepukana na Moto
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Hatoingia motoni yeyote atakayesali kabla ya kuchomoza juwa na kabla ya kuzama kwake.(yaani Sala ya Alfajiri na ya Alasiri)”
    Muslim

    Kuingizwa Peponi
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Atakayezisali (Sala za) ‘baridi mbili’- Alfajiri na Alasiri ataingia Peponi.”
    (Zimeitwa Sala za ‘Baridi mbili' kwa sababu joto hupunguwa nyakati za Alfajiri na Alasiri na hali ya hewa inakuwa na ubaridi ndani yake).
    Bukhari na Muslim

    Kuuangalia uso wa Mwenyezi Mungu mtukufu
    Na hii ni starehe kubwa kupita zote za huko Peponi.
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu, hapana kitakachokuzingeni msiweze kumuona. Kwa hivyo kama mtaweza msishindwe (na shetani) kusali kabla ya kuchomoza juwa na kabla ya kuzama kwake, basi fanyeni hivyo”
    Bukhari na Muslim

    Anakuwa katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu na chini ya ulinzi Wake
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Atakayesali Alfajiri (jamaa) yumo katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu.”
    Muslim

    Kushuhudia kwa Malaika mbele ya Mwenyezi Mungu kwa wanaosali
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Wanapishana kuja kwenu Malaika wakati wa usiku na wakati wa mchana. Wanajumuika wakati wa Sala ya Alfajiri na Sala ya Alasiri,kisha wanapopanda wale waliokesha kwenu, Mwenyezi Mungu huwauliza - juu ya kuwa ana juwa kila kitu juu yao; “Mumewacha waja wangu wakiwa katika hali gani?” Na wao hujibu; “Tuliwaacha wakiwa wanasali na tulipowaendea pia walikuwa wakisali.”
    Bukhari na Muslim

    Anayesali Ishaa na Alfajiri jamaa anapata thawabu sawa na aliyesali usiku kucha
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Mwenye kusali Ishaa jamaa sawa na aliyesali nusu ya usiku. Na mwenye kusali Alfajiri jamaa sawa na aliyesali  usiku kucha.”
    Muslim

    Anaepukana na sifa za wanafiki
    Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;
    “Hapana Sala nzito kwa wanafiki kupita Sala ya Alfajiri na Ishaa (jamaa), lau kama wangejuwa yaliyomo ndani yake, basi wangekuja (msikitini kuzisali) hata kwa kusota (kama hawawezi kutembea kwa miguu yao).”
    Bukhari na Muslim
     
    Na kutoka kwa Ibni Omar (RA) amesema;
    “Ilikuwa tusipomuona mtu akija kusali Alfajiri na Isha (msikitini) tukimdhania vibaya.”
    Ibni Khuzayma katika Sahihi yake

    No comments:

    Post a Comment

    Fashion

    Beauty

    Culture