Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) alizaliwa katika mji unaoitwa Aar uliopo
kandokando ya mto wa Furaat (Euphrates) Al Kufa
- Iraq.
Inajulikana kuwa Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) aliuhama mji huo na kuishi sehemu iliyokuwa ikiitwa Haraan na hatimaye
akahamia nchi ya Palastina na huko ndiko alikofanya makao yake ya kuufikisha
ujumbe alopewa na Mola wake.
Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) anawasili Misri
Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akifuatana na mkewe alikwenda kutembelea
nchi ya Misri, na huko alipokelewa na mfalme wa Misri aliyewaweka ndani ya
qasri yake, na usiku ulipoingia mfalme huyo alijaribu kumdhuru Bibi Sarah mke
wa Nabii Ibrahim (Alayhis salaam), lakini Mwenyezi Mungu alimkinga bibi huyo na
shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze kila anapojaribu kumsogelea.
Alipoona dalili za qudra ya Mwenyezi Mungu zikimlinda bibi huyo, mfalme
akaacha vitimbi vyake na kuamua kumpa Bibi Sarah zawadi, na zawadi hiyo ni binti
yake aitwae Hajarah, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti huyo
mumewe Ibrahim (Alayhis salaam).
Anarudi kwao
Ibrahim (Alayhis salaam) akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake
wawili, Bibi Sarah na Bibi Hajarah, na kutokana na mke mpya, Mwenyezi Mungu alimruzuku
mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismail, jambo lililomfanya Bibi Sarah awe na
wivu mkubwa juu ya mke mwenzake, na baada ya kuamrishwa na Mwenyezi Mungu
Subhanahu wa Taala, Nabii Ibrahim akamchukuwa Bibi Hajarah pamoja na mwanawe
Ismail aliyekuwa bado mchanga wakati huo, na kufunga nao safari ndefu kutoka
Palastina hadi nchi ya Hijazi (Saudia hivi sasa).
Anawasili Makka
Alipowasili Makkah penye bonde baina ya Safa na
Marwa mahali kilipo kisima cha maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo nyumba
ya Mwenyezi Mungu (Al Kaaba) ilikuwa ni sehemu iliyonyanyuka tu juu ya ardhi,
ikishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa
ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.
Hapakuwa na mtu anayeishi mahali hapo wala
nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja alipowaacha mkewe na mwanawe chini yake,
akawawekea birika la maji pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake,
kisha akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina.
Mama yake Ismail alipomuona mumewe akirudi na
kuwaacha mahali hapo walipopafikia baada ya safari ndefu iliyowachukuwa siku
nyingi njiani, mahali pasipo na mji wala kijiji. Hapakuwa na
hata dalili ya kuwepo mtu mahali popote karibu na hapo, akamfuata mumewe na
kumuuliza:
“Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?”
Akamuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabii Ibrahim (Alayhis
salaam) hakumjibu.
Mwisho Mama yake Ismail akamuuliza:
“Mwenyezi Mungu ndiye Aliyekuamrisha?”
Nabii Ibrahim akamjibu:
“Naam, ndiyo.”
Kwa imani iliyothibiti, kwa utiifu mkubwa na kwa
moyo uliosalimu amri, Bibi Hajarah akamwambia:
“Kwa hivyo Hatotupoteza”.
Hapo ndipo Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) alipogeuka na
kuianza safari ndefu ya kurudi Sham akimuacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo
na wa pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo mahali ambapo mkewe
hakuweza kumuona, Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) akageuka nyuma na kuomba dua
ifuatayo:
رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ
ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ
فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ
الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ
“Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi ya kizazi changu
(mwanangu Ismaili na mama yake Hajarah) katika bonde (hili la Makkah)
lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (ya Al Kaaba
utakayotwambia tuijenge).
Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Sala. Na ujaalie nyoyo za watu zieleke kwao (wapende kuja kukaa hapa ili
pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.”
Ibrahim – 37
Anaamrishwa amchinje mwanawe
Nabii Ibrahim alikuwa mara kwa mara akija
Makkah kuwazuru mkewe na mwanawe na hapana anayejuwa uhakika wa idadi ya ziara
hizo, isipokuwa wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.
Ya mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismail (Alayhis
salaam) na mwanawe akakubali kutii amri hiyo, na alipomlaza mwanawe kifudifudi
ili asiuone uso wake asije akamuonea huruma, na baada ya Ismail (Alayhis
salaam) kutoa shahada, na Ibrahim kusalimu amri kwa Mwenyezi Mungu huku
akijitayarisha kumchinja mwanawe, Mwenyezi Mungu akamfunulia Nabii Ibrahim (Alayhis
salaam) kuwa asimchinje mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.
Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliposema:
فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ. وَنَادَيْنَاهُ
أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ. قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي
الْمُحْسِنِينَ. إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلَاء الْمُبِينُ. وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ
عَظِيمٍ
“Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi
Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje).
Pale pale tulimwita; “Ewe Ibrahim;
Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao).” Kwa yakini hivi
ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Bila shaka (jambo) hili ni jaribio lililo
dhahiri, (mtihani ulio dhahiri).
Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu,”
As Saaffaat – 103-107
Mama yake Ismail na kisima cha Zamzam
Bibi Hajarah (Mama yake Ismail) akawa anakula zile tende alizowekewa na mumewe huku akimnyonyesha mwanawe, lakini haukupita muda
mrefu maji yakaanza kupunguwa na hatimaye kumalizika, na mwanawe alipoanza
kuona kiu, Bibi Hajarah akaanza kuhangaika huku na kule akimtafutia maji.
Akaliendea jabali lililokuwa karibu yake - ‘Jabal Safa’ – na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza kutizama huku na
kule akitafuta maji au msafara wa watu watakaokuwa na maji, lakini hakuona
kitu.
Akateremka na kuanza kutembea taratibu penye
bonde lililopo baina ya jabali Safa na jabali Marwa, na alipofika kati kati ya
bonde akaanza kukazana huku akiliendea jabali Marwa na kulipanda, na alipofika
kileleni akaanza kutizama huku na kule, lakini bila mafanikio yoyote.
Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) amesema:
“Hiyo ndiyo Saayi mnayotembea baina ya Safa na
Marwa.”
Bibni Hajarah aliendelea kufanya hivyo mara saba,
na alipokuwa akiliendea jabali Marwa akasikia sauti ngeni ikimsemesha. Alinyamaza
kimya ili aisikie vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika
amesimama mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa, huku akichimba kwa ubawa
wake mpaka maji yalipofurika, ndipo mamake Ismail alipoyaendea na kuanza kuyachota kwa mikono
yake huku akimnywesha mwanawe na kunywa yeye mwenyewe.
Alipokuwa akinywa na kumnywesha mwanawe,
Malaika akamwambia:
“Usiogope - hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Mwenyezi Mungu
itakayojengwa na mtoto huyu na baba yake."
Watu wa kabila la Jurhum
Hazikupita siku nyingi na mama yake Ismail
akajiwa na msafara wa watu wa kabila la Jurhum ambao asili yao ni kutoka Yemen
waliokuwa wasafiri waliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkah mbali na
hapo, na walikuja baada ya kuwaona ndege wakiruka sehemu aliyopo mama yake
Ismail wakasema:
“Bila shaka ndege hawa wameona maji”, na kwa
vile inajulikana kuwa sehemu zile si kawaida kupatikana maji, wakaamua kutuma watumishi
wakachunguze sehemu walipoonekana ndege, na walipokiona kisima cha maji ya
Zamzam wakarudi kuwajulisha wenzao walioamua kukiendea haraka sana, lakini
walipomuona mama yake Ismail na mwanawe wakamuomba wakae naye wakamwambia:
“Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?”
Mama yake Ismail akawaambia:
“Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.”
Wakasema:
“Tumekubali.”
Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) amesema:
“Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismail,
kwani alikuwa mwenye kupenda watu.”
Mwambie abadilishe kizingiti
Watu wa kabila la Jurhum wakateremka na
kuazisha maisha mepya mahali hapo, na Nabii Ismail (Alayhis salaam) akaishi
pamoja nao, akajifundisha kwao lugha ya kiarabu, akajifundisha kuwinda, na
alipokuwa mkubwa wakamuozesha mmoja katika binti zao.
Baada ya kuishi muda aloishi, mama yake Ismail akafariki dunia na Ismail akaendelea kuishi mahali hapo pamoja na watu wa
kabila hilo la Jurhum.
Nabii Ibrahim alikuja kumtembelea mwanawe katika ziara yake ya pili
lakini bahati mbaya hajamkuta nyumbani na badala yake
alimkuta mkewe, na alipomuuliza mahali alipo Ismail akamwambia:
“Ametoka kwenda kututafutia rizki.”
Nabi Ibrahim akamuuliza juu ya hali zao na
mwanamke akamjibu:
“Sisi ni wanadamu na hali zetu ni za dhiki na
shida.”
Akaendela kumshitakia hali zao, na Nabi Ibrahim
alipoondoka kurudi nchi ya Palastina akamwambia:
“Akirudi mumeo msalimie kisha mwambie abadilishe
kizingiti cha nyumba.”
Aliporudi Nabii Ismail (Alayhis salaam) alihisi kuwa jambo fulani limetokea nyumbani kwake, akamuuliza mkewe:
“Alikuja mtu hapa?”
Mkewe akajibu:
“Ndiyo, alikuja mzee mmoja na wasfu wake ni
hivi na hivi, akauliza juu yako na mimi nikamwambia ulipo, akaniuliza juu ya
hali zetu, nikamwambia kuwa sisi ni wanadamu na kwamba hali zetu ni za dhiki na
shida.”
Akamuuliza:
“Alikuusia jambo lolote?”
Akajibu:
“Ndiyo, alinambia ukija nikusalimie kisha nikwambie
ubadilishe kizingiti cha nyumba.”
Akamwambia:
“Yule alikuwa baba yangu na ameniamrisha
nifarikiane na wewe, kwa hivyo rudi kwa wazee wako.”
Baada ya kumtaliki mkewe wa mwanzo, Nabii
Ismail (Alayhis salaam) akaoa mke mwingine, na inasemekana kuwa alikuwa binti
wa Mudhaadh bin Amru aliyekuwa Sheikh wa kabila la Jurhum.
Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akaja tena kumtembelea mwanawe katika
ziara ya tatu, na safari hii hajamkuta pia, na
alipomuuliza mkewe akamwambia:
“Amekwenda kutuletea mahitaji yetu.” Na Ismail alikuwa mwindaji anayesafiri mara kwa
mara sehemu za mbali kwa ajili ya kazi yake hiyo na huchukuwa muda mrefu
safarini.
Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akamuuliza:
“Vipi hali zenu?”
Akajibu:
“Tumesitirika alhamdulillah tumo katika kheri
kubwa.”
Akawa anasema
hivyo huku akimshukuru Mwenyezi Mungu.
Nabii Ibrahim akamuuliza:
“Mnakula chakula gani?”
Akajibu:
“Nyama.”
Akamuuliza:
“Mnakunywa nini?”
Akajibu:
“Maji.”
Akamwambia:
“Mola wangu vibariki nyama na maji.”
Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu
alayhi wasallam): “Siku hiyo hawakuwa na chochote nyumbani kwao.”
Nabii Ibrahim akamwambia:
“Akirudi mumeo mpe salamu zangu na umwambie
akidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yake.”
Aliporudi Ismail akauliza:
“Alikuja mtu leo?”
Akajibu:
“Alikuja mzee mmoja mwenye umbo zuri, akataka
kujuwa habari zako, nikamjulisha, akaniuliza juu ya hali zetu nikamwambia kuwa
tupo katika kheri.”
Akamuuliza:
“Alikuusia jambo lolote?”
Akamwambia:
“Ndiyo, yeye anakupa salamu nyingi na anakwambia
ukidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yako.”
Akamwambia:
“Yule alikuwa baba yangu na ananiamrisha nikamatane
na wewe.”
Wananyanyua nguzo za Msikiti
Nabii Ibrahim akaja tena katika ziara yake ya nne,
na safari hii Ismail alikuwepo nje ya nyumba yake chini ya mti karibu na kisima
cha maji ya zamzam akichonga mshale wake, na alipomuona baba yake akamnyanyukia
kwa heshima kubwa, akamwamkia kama mtoto anavyoamuamkia baba yake wakakumbatiana
kisha Nabii Ibrahim akasema:
“Mwenyezi Mungu amenipa amri.”
Ismail akamwambia;
“Fanya kama ulivyoamrishwa na Mola wako.”
Akamwambia:
“Na wewe unisaidie.”
Akamwambia:
“Nitakusaidia.”
Akamwambia:
“Mwenyezi Mungu ameniamrisha nijenge nyumba mahali hapa..”
Akamuonesha ile sehemu ya ardhi iliyoinuka karibu na
kisima cha maji ya zamzam, kisha wote kwa pamoja wakaanza kufanya kazi ya
kuzinyanyua nguzo za nyumba na kuijenga Al Kaaba, na Ismail akawa anamsogezea
baba yake mawe huku Ibrahim akijenga, mpaka nyumba ilipokamilika. Walikuwa
wakijenga huku wakiomba dua ifuatayo:
“Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga
huu msikiti.”
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ
وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
“Na Ibrahimu alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al Kaaba) na Ismaili (pia) (wakaomba wakasema) “Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu msikiti.
Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.”
Ibrahim – 127
Na ِkasema:
رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو
عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ
إِنَّكَ أَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ
“Ee, Mola Wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao
awasomee Aya Zako, na kuwafundisha Kitabu (chako) na hikima (nyingine) na
awafundishe kujitakasa (na kila mabaya) hakika Wewe ndiye Mwenye, nguvu na
ndiye Mwenye hikima.”
Al Baqarah-129
Na hii ndiyo tafsiri ya hadithi ya Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) alipoulizwa juu ya mwanzo wa
amri yake akasema:
“Mimi ni dua ya baba yangu Ibrahim na bishara
ya ndugu yangu Issa alayhimu ssalaam.”
Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa baada ya kukamilisha ujenzi
wa msikiti wa Al Kaaba, Mwenyezi Mungu akamuamrisha
Nabii Ibrahim awatangazie watu waje kuhiji, na Nabii Ibrahim akasema:
“Ewe Mola wangu vipi itawafikia sauti yangu.”
Akamwambia:
“Juu yako ni kutangaza tu, na ni juu Yangu
kuifikisha,” ndipo Nabii Ibrahim alipopanda juu ya kilele cha mojawapo ya
milima ya Makkah na kupaza sauti yake akisema:
“Enyi watu mumefaridhishiwa Hija katika nyumba kongwe,” na tangazo hilo likamfikia kila kiumbe baina ya mbingu na
ardhi.
“Hamuoni kuwa watu wanauitikia mwito huo kutoka
katika kila pembe ya dunia? Na katika
riwaya nyingine; “Na wa mwanzo kuuitikia mwito huo
walikuwa watu wa Yemen."
Kisa cha Watu wa ndovu (As habul fiyl)
Abraha Mhabeshi aliyekuwa gavana wa Al Najashi
katika nchi ya Yemeni iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia wakati huo alikuwa
akiona wivu kila anapowaona waarabu wakifunga safari ndefu kwenda kuizuru Al
Kaaba, na kwa ajili hiyo akaamua kujenga kanisa kubwa kati ya mji wa Sana-a
(mji mkuu wa Yemen) kisha akawataka waarabu waache kwenda Makkah na badala yake
wakahiji penye kanisa lake.
Habari hizo zilimfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinanah,
aliyeamua kuingia kanisani nyakati za usiku na kulipaka mavi, jambo
lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa lenye idadi ya askari
wanaozidi elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili na yeye mwenyewe akiwa
juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al
Kaaba.
Alipokaribia Makkah, penye bonde la Muhsir baina ya Muzdalifa na Mina, tembo mkubwa akapiga magoti na kukataa kuendelea na
safari. Ikawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah
anakataa na hupiga magoti.
Wakawa katika hali hiyo mpaka pale Mwenyezi Mungu alipowapelekea ndege
makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo
unaounguza.
Mwenyezi Mungu Anasema:
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِأَصْحَابِ الْفِيلِ.
أَلَمْ يَجْعَلْ كَيْدَهُمْ فِي تَضْلِيلٍ. وَأَرْسَلَ عَلَيْهِمْ طَيْرًا
أَبَابِيلَ. تَرْمِيهِم بِحِجَارَةٍ مِّن سِجِّيلٍ. فَجَعَلَهُمْ كَعَصْفٍ
مَّأْكُولٍ
“Je! Huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wenye ndovu?
Je! Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika.
Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi
Wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma.
Akawafanya kama majani yaliyoliwa (yakatapikwa)?”
Suratul Fiyl
Ndege walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa
makundi, mfano wa vijumba mshale au zuwarde, kila mmoja akiwa amebeba mawe
matatu yenye ukubwa kiasi cha dengu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni,
na kila anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kufa.
Si wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo
wachache walioachwa wakarudi mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Ama
Abraha, Mwenyezi Mungu alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake
kukatika na kupukutika huku akirudi alikotoka, na
alifariki alipowasili mji wa Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku
aliyenyonyoka manyoa.
Makureshi, wao walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na
hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kumalizika yaliyotokea.
Tukio hili lilitokea mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) kwa siku hamsini au hamsini na
tano takriban muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo wa mwezi wa March
mwaka 571 baada ya Nabii Issa.
Katika tafsiri ya Suratul Fyl anasema Ibni Kathiyr;
“Hii ni mojawapo ya neema za Mwenyezi Mungu
walizopewa Makureshi baada ya kuwalinda na shari walهokuja nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al Kaaba
na kuiondoa ili isiwepo tena. Lakini Mwenyezi Mungu aliwaangamiza na kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa juu ya
kuwa walikuwa watu wanaofuata dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa
bora kuliko Makureshi waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni
matayarisho ya kuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam),
kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule alizaliwa.
Kama kwamba uhakika wa mambo unasema; ‘Enyi
Makureshi hamkupata nusura hii juu ya Mahabeshi kutokana na ubora wenu, bali
kwa ajili ya kuilinda nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi
karibuni kwa Mtume wa Mwenyzi Mungu, Muhammad (Swalla Llahu alayhi wasallam)
mwisho wa Manabii."
Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na
kwa vile Wahabeshi walikuwa na uhusiano mzuri na ًWarumi, Waajemi waliokuwa wakingoja fursa nzuri kama hii wakaingia na
kuiteka nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Uajemi na Roma)
ndizo zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la
kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa nyumba
ile ya Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeitukuza na kuiadhimisha,
na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake akasema kuwa yeye ni
Mtume, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo.
Kwa hivyo ndani ya tukio hili mna hekima iliyojificha ya Mwenyezi Mungu
ya kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani
kwa njia ya kimiujiza.
Kuijenga upya Al Kaaba
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) alikuwa na umri
wa miaka thelathini na tano wakati Makureshi walipoujenga upya msikiti wa Al
Kaaba, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabi Ismail alipoujenga na
hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundu la udongo lenye urefu
wa kiasi cha dhiraa sita, bila ya kipaa, jambo lililowarahisishia wezi kuingia
ndani na kuiba hazina zinazowekwa humo.
Na kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea
kujengwa kwake, kanuni za maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka mitano kabla ya kupewa utume (Swalla
Llahu alayhi wasallam) yalitokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia
ndani ya msikiti na kubomoa sehemu kubwa za msikiti huo, na kwa ajili ya yote
hayo Makureshi wakaamua kuujenga tena msikiti huo.
Wakakubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa
jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari
ya mzinzi, wala pesa za riba, wala pesa alizodhulumiwa mtu nk.
Walikuwa wakiogopa kuubomoa msikiti na kuanza
kuujenga upya wasije wakadhurika, mpaka alipotangulia Al Walid bin Mughiyrah na
kuianza yeye kazi hiyo, na wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo
nao wakaingia kazini. Wakawa wanaendelea kuubomoa mpaka walipozifikia nguzo
zilizosimamishwa na Nabii Ibrahim (Alayhis salaam),
kisha wakaanza kuujenga upya msikiti huo, na kila kabila likapewa sehemu yake
ya kujenga, na kila kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na
msimamiaji wa ujenzi alikuwa Mrumi aitwae Baqum.
Kazi ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa
kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, ndipo mzozo ulipoanza kila kabila likataka
kupewa heshima hiyo ya kulirudisha mahali pake.
Mgogoro uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu hata
watu wakakaribia kutaka kupigana vita, panga mkononi mpaka pale Abu Umayyah bin
Mughiyra Al Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia msikitini kupitia
mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na rai hiyo.
Mwenyezi Mungu akataka Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wasallam)) awe
mtu huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja
wakapiga ukulele wa kuridhika:
"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye, huyu
Muhammad."
Alipojulishwa juu ya uamuzi huo, Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) (hii ilikuwa kabla ya kupewa
utume) alikubali, na kwa utulivu akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na
kuliweka jiwe jeusi juu yake, kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila
mmoja akamate upande wa kitambaa, kisha wanyanyuwe kwa pamoja. Wakalinyanyua na walipopafikia mahali pa kuliweka, Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llahu alayhi wasallam)) akalinyanyua yeye kwa mikono yake miwili na
kulirudisha mahali pake.
Kwa njia hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wasallam) aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji
wa damu mkubwa baina ya Makabila ya Kikureshi, na kila mmoja aliondoka hapo
akiwa ameridhika.
Wanaishiwa na pesa za halali
Makureshi walishindwa kuukamilisha msikiti baada ya kuishiwa na pesa za halali, wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita
upande wa kaskazini mwa Al Kaaba na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la
Al Hijr (Hijr Ismail) wakashindwa kuunganisha msikiti pamoja na Hijri Ismail
ambayo asili yake ilikuwa imekamatana na msikiti. Wakaunyanyua mlango kiasi cha
dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi asiweze kuingia isipokuwa wanayemtaka wao tu,
na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi na tano wakaezeka sakafu juu
ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi hiyo, Al Kaaba ikawa na umbo la
mraba lenye urefu wa mita kumi na tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na
upande wa pili yake (mkabala wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu
wa mita kumi.
Na jiwe jeusi liliwekwa juu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya
ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa mita
kumi kila upande, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili kutoka juu ya
ardhi, na upande wa nje ya Al Kaaba ikaachwa ikiwa imezungukwa na msingi
ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo mita na upana wa kiasi cha nusu
mita.
Na sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash Shadherwan, sehemu ambayo asili yake
ilikuwa ndani ya jengo la Al Kaaba, lakini Makureshi iliwabidi waiache sehemu
hii bila kuijenga, na kwa ajili hiyo msikiti ukawa na umbo
la mraba badala ya umbo lake la asili lililofanana na herufi D iwapo
utaunganishwa na Hijr kama ulivyojengwa na Nabi Ibrahim (Alayhis salaam).
Mara ngapi umebomolewa na kujengwa upya?
Inajulikana kuwa Msikiti wa Al Kaaba umejengwa
kwa mara ya mwanzo na Nabi Ibrahim (Alayhis salaam).
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ
وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
“Na Ibrahimu alipoinua kuta za
nyumba (hii ya Al Kaaba) na Ismaili (pia) (wakaomba
wakasema) “Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu
hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.”
Ibrahim – 127
Imesimuliwa na Imam Muslim katika Sahihi yake
na pia ndani ya vitabu vyengine mbali mbali vya elimu ya hadithi na vya sira
katika mlango ya 'Kubomolewa na kujengwa upya msikiti wa Al Kaaba' kama
ifuatavyo:-
Sehemu kubwa ya msikiti iliungua wakati Al Hajjaj alipoushambulia
akitumia 'Manjaniq' (mtambo wa kutupa mawe uliokuwa ukitumika katika vitani vya
zamani) akitaka kumuuwa Abdullah bin Al Zubair bin Awaam (Radhiya Llahu anhu)
na hii ilikuwa wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiyah.
Mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu)
aliuacha msikiti kama ulivyo mpaka ulipoingia msimu wa Hija wa mwaka ule na
watu wakawa wengi, akawakusanya na kuwahutubia, akasema:
"Enyi watu! Nataka ushauri wenu juu ya Al Kaaba. Niuvunje msikiti wote kisha niujenge upya au nitengeneze tu sehemu
zilizoungua?"
Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) akasema:
"Mimi ninayo rai, naona ni bora usiubomoe,
bali utengeneze tu na uiache kama ilivyo nyumba waliosilimu watu juu yake, na
mawe waliosilimu watu juu yake, na alitumwa kwa ajili yake nyumba hiyo Mtume (Swalla
Llahu alayhi wasallam)."
Mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu) akasema:
"Mmoja wenu ikiungua nyumba yake hatoridhika
kuiacha ilivyo (bila shaka atapenda kuijenga upya), vipi basi nyumba ya Mola
wenu? Mimi nitaswali Istikhara mara
tatu kisha nitaamua."
Na baada ya kukamilisha tatu akaamua kuubomoa, lakini kila mmoja
aliogopa kupanda na kuianza kazi hiyo asije akadhurika, mpaka alipopanda mtu
mmoja na kunyanyua jiwe, akalitupa chini, na watu walipomuona hajadhurika
wakaingia na wao kazini na kuianza kazi ya kuubomoa msikiti mpaka walipozifikia
nguzo, kisha mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu) akazinyanyua nguzo na
kuujenga upya, na alipomaliza akaishonea Al Kaaba pazia, akaujenga msikiti kama
ulivyokuwa wakati wa Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) kisha akasema:
"Nilimsikia khale yangu (Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) akisema
kuwa amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu
alayhi wasallam)) akisema:
"Ingelikuwa watu hawakutoka hivi karibuni tu katika ujahilia na ningelikuwa na pesa za kutosha kuujenga vizuri msikiti,
ningeongeza dhiraa tano na kuuganisha na Hijri (Ismail) kisha nikajaalia mlango
kwa ajili ya watu kuingia ndani yake na mlango wa kutokea."
Na katika riwaya nyingine:
"Makureshi walipoijenga nyumba walishindwa
kuikamilisha kwa sababu waliishiwa na pesa."
Na katika riwaya nyengine kupitia kwa Abdullah
bin Abubakar (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu
alayhi wasallam)) alisema:
"Na ningejenga milango miwili, mmoja mashariki na
mmoja magharibi ikawa juu ya ardhi kisha ningeunganisha msikiti na Hijri
Ismail."
Akasema Abdullahi bin Zubair (Radhiya Llahu anhu):
"Mimi leo ninazo pesa na siwaogopei
watu."
Akaongeza dhiraa tano na akajenga milango
miwili, mmoja kwa ajili ya watu kuingia na mwengine wa kutokea.
Inajengwa tena
Alipouliwa Abdullahi bin Al Zubeir (Radhiya Llahu anhu), Al Hajjaj
akamuandikia Abdul Malik bin Marawan aliyekuwa Khalifa wa
Waislamu wakati huo na kumjulisha juu ya mabadiliko aliyofanya mwana wa Al
Zubair katika msikiti, na Abdul Malik akamjibu:
"Urefu alouongeza mwana wa Al Zubair uache
na sehemu aloongeza katika Hijri ibomowe na milango aloiongeza izibe."
Al Hajjaj akafanya kama alivyoambiwa.
Hitimisho
Riwaya zinazokubalika zilizopokewa na maulamaa
zinasema kuwa msikiti umejengwa mara nne.
Ya kwanza ulipojengwa na Nabi Ibrahim (Alayhis
salaam).
Ya pili wakati wa ujahilia kabla ya Uislamu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llahu alayhi wasallam)) alishiriki katika ujenzi huo na wakati huo alikuwa na
umri wa miaka thelathini na tano na katika riwaya nyingine alikuwa na umri wa
miaka ishirini na tano.
Ya tatu ulipojengwa na mwana wa Al Zubair (Radhiya
Llahu anhu).
Ya nne ulipojengwa tena na Al Hajjaj baada ya
kupewa amri na Abdul Malik bin Marawan ya kubomoa zile sehemu zilizoongezwa na
mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu).
Imepokelewa pia kuwa Harun Al Rashid alitaka ushauri wa
kuujenga upya msikiti huo na kuzirudisha zile sehemu zilizojengwa na Abdullah
mwana wa Zubair (Radhiya Llahu anhu), lakini Imam Malik akamnasihi kwa
kumwambia:
"Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ewe amiri wa
Waisalamu, tafadhali iache nyumba kama ilivyo, na usiifanye ikawa mchezo kwa
wafalme, kila mmoja akaja kubomoa na kuujenga upya atakavyo, na mwisho wake
haiba ya nyumba itaondoka ndani ya vifua vya watu."
Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Ndugu yenu
No comments:
Post a Comment