Hiki
ni kisa cha kusikitisha, cha kufundisha na cha kuzingatia na kinaanzia
kwa aliyekuwa mumewe Yaasir. Yaasir akiwa pamoja na ndugu zake wawili walitoka Yemen kuelekea Makkah kwa lengo la kumtafuta ndugu yao aliyepotea kwa miaka mingi.
Jitihada
yao haikuweza kuzaa matunda na baada ya kuchoka wakaamua kurudi kwao
Yemen isipokuwa Yaasir ambae alipendezewa sana na mji wa Makkah na
akaamua kubakia hapo.
Ilikuwa
ni kawaida ya wageni kutafuta mwenyeji wa kumpa himaya na hivyo Yaasir
akapatiwa himaya na Abu Hudhayfah ibn Al Mughiyrah Al Makhzuumiy ambae
alikuwa na kijakazi aliyekuwa akiitwa Sumayyah.
Baada
ya kupita muda Sumayyah aliolewa na Yaasir na wakapata mtoto wao wa
kwanza aliyeitwa ‘Ammaar. Abu Hudhayfah alimwachia huru kijakazi wake
Sumayyah na wakaendelea kuwa na mahusiano mazuri kati yao. Pia
walijaaliwa watoto wengine wawili Abdullah na Harith. Abdullah alifariki
kabla ya kuja Uislamu.
Ilipotangazwa
dini ya haki iliyovunja ibada za kijahiliya katika mji wa Makkah na
kuletwa kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam, ni watu wachache katika
mji wa Makkah waliothubutu kusilimu. Miongoni mwao alikuwa ni Sumayyah.
Kwa mujibu wa nukuu za kihistoria anasemekana ni mtu wa saba kusilimu.
Alisilimu yeye pamoja na mumewe na mtoto wao ‘Ammaar.
Kusilimu
kwao wakati wakihesabika kuwa wageni kwa kukosa nasaba inayojulikana,
familia ya mama Sumayyah ilikuwa katika wakati mgumu.
Kutoka
kwa Mujahid anasema: Wa kwanza kudhihirisha Uislamu ni saba. Mtume
Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam, AbuBakr, Bilaal, Khabaab, Suhayb, ‘Ammaar
na Sumayyah . Ama Mtume Salla Allahu ‘Alayhi alihamiwa na Ami yake Abu
Talib. Abu Bakr ilimhami kaumu yake na adhabu, wakachukuliwa wengine na
kuvishwa minyororo ya chuma na kupelekwa kwenye jangwa , jua likiwaka na
kuteswa haki ya kuteswa….
Aliposikia
Abu Jahl kusilimu kwao pia alikwenda kuwatesa Sumayyah, mumewe na mtoto
wao ‘Ammaar kwa kuwapiga wote. Ikumbukwe Sumayyah alikuwa tayari ni mtu
mzima. Watu walikuwa wakipita kushuhudia mateso waliyokuwa wakiyapata
kwa kulazwa chini kwenye mchanga umoto, huku wakipigwa na jua kali la
jangwani kufikia kuzimia na wakiamka tu mateso huendelea wakitakiwa
kuikana dini mpya na kurudi katika kuabudu masanamu.
Siku moja alipita Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam sokoni na
kuona ukatili wa Maquraysh walipokuwa wakiwatesa familia ya Yaasir.
Lakini hakuweza kufanya chochote kwa kutokuwa na uwezo na aliwaombea
du’aa kwa kusema:
أَبْشِرُوا آلَ عَمَّارٍ ، وَآلَ يَاسِرٍ ، فَإِنَّ مَوْعِدَكُمُ الْجَنَّةُ "المستدرك(5666) صحيح
“Nnawabashiria Enyi Ukoo wa ‘Ammaar na ukoo wa Yaasir. Hakika miadi yenu ni pepo.” Al Mustadrak – Sahih
Ni katika kipindi hiki Waislamu dhaifu wasiokuwa na himaya au kinga kutoka kwa Maquraysh walipata taabu sana kama kina Bilaal, Suhayb, Khabaab na wengineo.
Jaribu
kufikiria aina ya mateso aliyoyapata Sumayyah ambae ni mwanamke mtu
mzima na jinsi alivyokataa kubadilisha imani yake na kuiuza dini yake.
Siku
moja alipita Abu Jahl karibu na sehemu waliyokuwa wakiendelea kuteswa
na kumsikia Sumayyah akilirudia neo la Tawhiyd – Ahad Ahad – mmoja,
mmoja, Allahu Akbar, Allahu Akbar – Mwenyezi Mungu ni mkubwa Mwenyezi
Mungu ni mkubwa. Abu Jahl , kwa hasira na ghadhabu, alimuamrisha
amkufurishe Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Sumayyah alimkatalia.
Na alipokuwa anamkaribia alijikongoja kwa nguvu chache alizokuwa nazo na
kumtemea mate Abu Jahl usoni.
Si
kitu alichokitarajia kufanyiwa sayyid wa Maquraysh na mama huyu aliye
chini akiugua kwa mateso na adhabu. Ghadhabu zilimpanda Abu Jahl na
kuchukua mkuki ambao alimchoma Sumayyah na kufariki hapo hapo. Sumayyah
alikuwa ni Muislamu wa mwanzo kufa shahidi.
Licha
ya kuwa dhaifu, licha ya kutokuwa na nasaba ya kumlinda,Sumayyah
alisalimisha maisha yake kwa Allah Subhaanahu Wata’ala na Mtume wake
Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Hakukubali kumsaliti Mola wake wala
kumsaliti Mtume wake. Licha ya kwamba ndiyo kwanza Uislamu unaanza,
Sumayyah alionesha na kuwawekea Waislamu msingi na maana ya kushikamana
na kujenga msimamo madhubuti katika dini. Ni msingi huu ambao Allah
Subhaahau Wata’ala anatukumbusha katika Quraan kwa kusema Attawbah /111
إِنَّ
اللّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ
لَهُمُ الجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيَقْتُلُونَ
وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ
وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللّهِ فَاسْتَبْشِرُواْ
بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
Hakika
Allah amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata
Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allah - wanauwa na wanauwawa. Hii ni
ahadi aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Quraan. Na
nani atimizae ahadi kuliko Allah? Basi furahini kwa biashara yenu
mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
Alipouawa Abu Jahl katika vita vya Badr , Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alimwambia ‘Ammaar bin Yaasir kwamba:
قتل الله قاتل أمِّك"“
“Allah amemuua (leo) aliyemuua mama yako”
Sumayyah
ni mfano wa kuigwa katika kusadikisha yale waliyoahidi kwa Mola wao
litokee lenye kutokea. Ni mfano mwema wa kujifundisha nini maana ya
kujiweka katika msimamo imara usiotetereka katika dini. Amesadikisha
Allah Subhaanahu Wata’ala aliposema Al Ahzaab/23
مِنَ
الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ
فَمِنْهُم مَّن قَضَى نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا
تَبْدِيلًا
Miongoni
mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Allah. Baadhi yao
wamekwishakufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata
kidogo.
No comments:
Post a Comment